Hali ya sintofahamu imezidi kuiandama klabu ya Chelsea, kumekuwa na matukio ambayo hayaeleweki toka msimu umeisha lakini kipigo cha juzi kutoka kwa Burnley kimezidi kuchafua hali ya hewa ndani ya Chelsea.
Kama unakumbuka wiki chache baada ya dirisha la usajili ndani ya Chelsea kufunguliwa kuliibuka tetesi kwamba Antonio Conte amechukizwa na sera za usajili wa Chelsea hali iliyofikia kutaka kuondoka.
Moja ya malalamiko ya Conte ilikuwa ni kukosa userious katika suala la usajili jambo ambalo lilipelekea kukosa wachezaji awatakao akiwemo Romelu Lukaku na pia Conte akitaka kupewa nafasi kubwa zaidi katika maamuzi.
Maisha yakaendelea na Conte akasaini mkataba mpya lakini wiki hii suala hilo limejitokeza tena na taarifa zinasema hali sio shwari hata kidogo kati ya klabu ya Chelsea na Muitaliano huyo baada ya Conte kudai mabosi wanamuangusha.
Wachambuzi mbali mbali wa masuala ya soka barani Ulaya wameshaanza kutabiri kwamba huu ni msimu wa mwisho wa Conte huku wacheza kamari nao wakianza kubet kwamba Conte anaweza asimalize msimu huu wa ligi.
Wakati Conte akianza kutabiriwa kuondoka Chelsea kwingineko mshambuliaji aliyeko kwenye msuguano na kocha huyo Diego Costa ametakiwa kurejea klabuni hapo ili kujiunga na wenzake kwa ajili ya msimu wa ligi.
Itambulike kwamba Costa bado ni mchezaji wa Chelsea na bado ana mkataba nao hivyo klabu yake imeamua kumrejesha kikosini japo anatakiwa kwanza kuanza kufanya mazoezi na wachezaji wa akiba.
Diego Costa mwenyewe kuhusu kufanya mazoezi na timu ya wachezaji wa ziada amesema “sio sawa kwa sababu mimi sina tatizo na mimi sina kosa kama ni faina sawa tu acha wanikate”. Hadi sasa haijafahamika wazi kwamba Costa atabaki Chelsea au atapata timu mpya kama anavyotaka.
Post a Comment