Taifa Stars – timu ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa mwaka 2017 inaingia uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya kalenda ya FIFA.
Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeatangaza kushusha bei ya kiingilio kwa watu watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.
“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio vya bei ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia gharama kidogo kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,” ameagiza Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu watakaoketi Majukwaa Maalumu – VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi VIP “B” na “C” watalipia Sh 10,000.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake aliwathibitishia Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.
“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu.
Kwa upande wa Peter Buffler – Kocha Mkuu wa Botswana, alisema kwamba anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa kikosi cha Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu. Mchezo ambao pia ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.
Post a Comment