BANDA SIMAMISHWA KUCHEZA LIGI KUU TANZANIA BARA



Beki wa Simba, Abdi Banda amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla wakati akiwa hana mpira kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF


Abdi Banda
Banda anadaiwa kufanya kitendo hicho ambacho hakikuonwa na waamuzi katika mechi kati ya Kagera Sugar na Simba iliyofanyika Aprili 2, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. 
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya kitendo cha aina hiyo kwenye mechi kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
"Kwa vile kosa hilo ni la kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo". Imesema sehemu ya taarifa ya TFF kwa wanahabari.
Kadhalika Klabu ya Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post